Waziri Wa Ulinzi Na Jeshi La Kujenga Taifa Azindua Jengo La Taasisi Ya Utafiti Wa Afya Zanzibar

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Ali Hassan amesema tafiti za kisayansi za Afya zinasaidia kujua chanzo cha maradhi na tiba yake ikiwemo matumizi ya dawa asilia.

Dk.Husein ameeleza hayo Binguni Wilaya ya Kati Unguja wakati wa Ufunguzi wa Jengo la Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI) ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Hassan akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa Jengo la Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI), katika kijiji cha Binguni Wilaya ya Kati, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema tafiti za kisayansi ya afya katika nchi zinamchango mkubwa katika kupunguza maradhi kwani baadhi ya maradhi yanaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia vyakula vya kawaida bila kutumia dawa za Hospitali.

Amewataka wananchi kupokea matokeo ya tafiti zitakazofanywa na Taasisi hiyo na Taasisi nyengine ili kuleta mabadiliko katika maisha yao.

Dkt. Hussein aliwashauri wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar kufanyakazi kwa juhudi na maarifa na  kuhakikisha mimea na dawa za asili zinazotumika kuwa ziko katika hali ya usalama kwa matumizi ya binaadamu.

Ameeleza kuwa shabaha ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kumkomboa mwananchi na madhila mbali mbali yakiwemo maradhi na kuwafanya wawe na afya bora.  

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla amesema lengo la kuanzishwa Taasisi hiyo ni kufanya tafiti kujua ukubwa na chanzo cha maradhi na kushirikiana na Taasisi nyengine kutoka nje ili kupata tiba sahihi. .  

Amesema zaidi ya shiling million mia mbili zimetumika katika ujenzi wa jengo la Taasisi ya Utafiti ya afya Zanzibar lenye wafanyakazi 21 na mipango ya kuajiri wataalamu wa fani ya utafiti zinaendelea kuchukuliwa ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.