Halmashauri ya wilaya ya kusini Unguja imesema imefanikiwa kutekeleza dhana ya ugatuzi kwa vitendo ikiwemo kuandikisha wanafunzi wanaotarajiwa kuanza Elimu ya maandalizi kwa asilimia 70.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya kusini Unguja Kassim Abou Mtoro alisema Elimu ya maandalizi na msingi imo katika orodha ya mambo yaliyogatuliwa kwenda katika Serikali za mitaa.

Alisema wamefanikisha kuandikisha wanafunzi kuanza Elimu ya maandalizi baada ya kuwahamasisha wazazi kufahamu malengo ya Serikali na umuhimu wa Elimu hiyo.

‘’Tumo katika kutekeleza ugatuzi kwa muda wa miaka miwili sasa ambapo mafanikio makubwa yamepatikana katika upande wa Elimu ya maandalizi na msingi kwa kuandikisha idadi kubwa wa watoto’’alisema.

Alisema kwa sasa wanakabiliana na baadhi ya  changamoto  ikiwemo uhaba wa madarasa kufuatia wingi wa wanafunzi walioitikia wito kuanza Elimu maandalizi.

‘’Halmashauri ya Wilaya ya kusini kwa sasa tunapambana na tatizo la uhaba wa madarasa kufuatia wingi wa wanafunzi wanaotarajiwa kuanza Elimu ya maandalizi’’alisema.

Mwalimu wa shule ya Kitogani Salama Ali alisema wamepokea idadi kubwa ya wanafunzi wanaotarajiwa kuanza Elimu ya maandalizi ingawa tatizo ni uhaba wa madarasa.

Aliwapongeza wazazi kwa kuitikia wito wa kuleta watoto wao kuanza Elimu ya maandalizi ya miaka miwili na baadaye kuanza Elimu ya msngi darasa la kwanza.

Mmoja ya wazazi aliyejitambulisha kwa jina la Mwaka Jecha alisema wamepewa Elimu ambayo imewashajihisha vya kutosha umuhimu wa kupeleka watoto kuanza Elimu ya maandalizi ikiwa ni moja ya sera ya Wizara ya Elimu.

’Tulipewa Elimu kuhusu umuhimu wa kuwapeleka watoto kuanza Elimu ya maandalizi katika mradi wa (PAZA) unaotekelezwa na chama cha waandishi wa habari za maendeleo (WAHAMAZA) ambao ulikuwa na lengo la kujenga uwezo kwa wananchi kuweza kushiriki shughuli za maendeleo’’alisema.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza Elimu ya maandalizi kuwa ya lazima ikiwa na lengo la kumpa mtoto uzoefu wa kujuwa kusoma na kuandika kabla ya kuingia katika Elimu ya msingi.