Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema itaendelea kusimamia utekelezaji wa matakwa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufikia malengo yaliyokusudiwa ili kuwasaidia Vijana .

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Balozi Ali Karume, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Amour Hamil Bakari  katika kikao cha tatu kwa Mwaka wa Bajeti 2018-2019 cha Baraza la Watendaji huko Ukumbi wa Bassfu Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar amesema Wizara inaendelea kuratibu masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya Vijana kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi.

Alisema Baraza la Watendaji linapaswa kuwajibika ipasavyo ili kujenga uhusiano mzuri na mabaraza ya vijana kwa kuwakomboa katika vitendo viovu vinavyo athiri na kupoteza mwelekeo wa maisha.

“Baraza la Watendaji mnapaswa kuwajibika ipasavyo ili kujenga uhusiano mzuri na mabaraza ya vijana kwa kutimiza lengo lililokusudiwa kuanzishwa mabaraza hayo”alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Alifahamisha kuwa uwepo wa Baraza la Watendaji ni kusimamia na kuratibu kazi za kila siku za baraza, kutekeleza maadhimio yaliyowekwa na mkutano Mkuu wa Taifa, kupokea na kufanya mapitio na kupitisha mipango ya muda ya bajeti na taarifa.

Pia Baraza hilo linaweza kutathmini utekelezaji wa mipango na kuandaa taarifa za utekelezaji kwa mkutano mkuu Taifa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuleta maendeleo.

Aidha alieleza kuwa kufanyika kwa vikao vya  Watendaji kunasaidia kupata mbinu mbalimbali za utekelezaji na kuweza kutathmini  malengo ya kazi zao na kuleta ufanisi mzuri katika utendaji wao ili kuleta maendeleo kwa vijana na Taifa

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Faraji Abdalla alisema lengo la Kikao cha tatu kwa Mwaka wa Bajeti 2018-2019 cha Baraza la Watendaji ni kufanya tathmini na kupitia taarifa za mpango kazi wa mwaka huo ili kuleta mafanikio kwa vijana.

Alisema kuwa Baraza lake limeweka mikakati madhubuti ya kuwahamasisha vijana kujiunga na mabaraza ya vijana kutumia njia mbali mbali ikiwemo kufanya ziara katika Shehia, Skuli na Vyuo vikuu, Makongamano tofauti ya Vijana pamoja na kutumia mitandao ya Kijamii.

Na: Maryam Himidi Kidiko.