Vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, klabu ya Yanga, imeweka wazi kuwa haina mpango wa kumsajili kiungo wa zamani wa Simba ambaye kwasasa anaichezea African Lyon Haruna Moshi maarufu ‘Boban’.

Akiongea na www.eatv.tv Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Yanga Hussein Nyika, amesema hawajamsajili na wala hawana mpango wa kumsajili kiungo huyo wakati huu wa dirisha dogo.

”Ni kweli kocha wetu Mwinyi Zahera amemsifia sana Boban kuwa kiwango chake kimeimarika lakini haimanishi kuwa tunamsajili au tumeshamsajili”, amesema Nyika.

Boban ambaye amewahi kuchezea vilabu vya Simba, Mbeya City pamoja na Gefle ya nchini Sweden amekuwa akicheza kwa kiwango bora akiwa na African Lyon ambapo aliisaidia kupanda ligi kuu na sasa anaendelea nayo vizuri kwenye ligi.

Nyika amesisitiza kuwa mwalimu Zahera bado hajapendekeza kuongezewa wachezaji na kama atahitaji basi watasajili. Zahera hivi karibuni alisema hatafanya usajili kwani wachezaji waliopo bado wana madai mengi hivyo hawezi kuongeza wengine.