Viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Zanzibar (ZAA) na Mamlaka ya Uendelezaji wa Viwanja vya Ndege Kilimanjaro (Kadco), wameeleza sababu ya kusudio la  kuanzisha tozo mpya katika viwanja hivyo.

Miongoni mwa sababu hizo ni gharama kubwa za uendeshaji katika kukabiliana changamoto ya ulinzi na usalama.

Wameeleza hayo leo Alhamisi Aprili 11, 2019 wakati kikao cha wadau wa sekta ya anga kilichojadili maombi ya tozo hiyo kilichofanyika ofisi ya makao mkuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Ufundi wa Kadco, Martin Kinyamagoha amesema gharama za uendesha zimekuwa kubwa na wamelenga kuimarisha ulinzi na usalama wa viwanja vya ndege na abiria kwa kununua vifaa vya kisasa zaidi vya ulinzi.

Kinyamagoha amesema licha ya kununua baadhi ya mashine  zikiwamo kamera na mashine za utambuzi, wana mpango  wa kuagiza nyingine sita ili kuimarisha uwanja huo.

Abiria atalipia tozo hizi moja kwa moja wakati wa ununuzi wa tiketi. Tumelenga kukabiliana hali ya ulinzi na usalama kutokana na teknolojia kukua,” amesema Kinyamagoha.

Naye Mkurugenzi wa ZAA, Zaina Ibrahim Mwalukuta, amesema tozo hizo zitasaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Aman Abeid Karume na kuvutia baadhi ya mashirika ya ndege kushusha na kupakia mizigo visiwani humo.

“Sasa hivi baadhi ya mashirika makubwa ya ndege yamekataa kushusha na kupakia mizigo kwa sababu uwanja hauna mashine ya X-ray ya kukagua mizigo hiyo. Mashirika haya hayataki mizigo yao ifunguliwe badala yake, wanataka ipitishwe katika mashine maalumu ya ukaguzi,” amesema Zaina.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema mamlaka hiyo ina wajibu wa kuhakikisha mifumo ya ulinzi na usalama inakuwa imara ili kuzuia watu wenye nia ovu kupenya katika viwanja vya ndege.

“Ndiyo maana mtu au mamkala ikija na wazo kama hili linalolenga kuimarisha ulinzi tunaliona la maana. Tutajadiliana hapa kwa wadau kutoa maoni yao na mwisho TCAA itakuwa kama hakimu kuhusu jambo hili,” amesema Johari.

Johari amesema sekta ya anga inazidi kukua na baadhi ya mashirika yameonyesha nia kuanza safari katika soko la kimataifa ikiwamo Marekani.

“Sasa ili tufanikiwe kikamilifu kuyapata masoko hayo, lazima wenzetu waje kukagua na kujiridhisha na mifumo ya ulinzi na usalama katika viwanja vyetu vya ndege hasa vya kimataifa,” amesema Johari.