Halmashauri ya Wilaya Bukoba ipo mbioni kuanza kutekeleza na  kujenga Miundo mbinu ya Kudumu ya mradi mkubwa wa kusambaza Maji katika Chuo kipya cha Ufundi stadi  VETA kinachotarajiwa kujengwa katika Kijiji cha Burugo, Kata Nyakato mradi  utakaogharimu zaidi ya Milioni 900.

Akizungumza na wanahabari Ofisini kwake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba, Murshidi Ngeze ameeleza kuwa Mchakato wa kupata mkandarasi tayari umefikia hatua nzuri baada ya zile taratibu za awali kukamilika ambazo ni pamoja na kutangaza zabuni, na tayari Kamati ya fedha imejadili na hivi karibuni itamtangaza Mkandarasi ambae baada ya kutiliana saini ataanza kusambaza kazi ya Ujenzi wa mradi wa Maji katika Chuo hicho, ambapo pia utavinufaisha  Vijiji jirani vinavyopakana hapo.

Awali Halmashauri ya Bukoba  ilipeleka mradi wa  Maji ya awali ya kuanzia yaliyogharimu zaidi ya Milioni 19, ambapo fedha hizo zilitokana na mapato ya Ndani.

Ujenzi wa mradi huu utashirikisha pia wakazi wa eneo husika katika maana ya (Force Account), hivyo wakazi wa eneo hilo watahusishwa katika kazi ndogondogo.