Zanzibar na wimbi la uingizwaji wa bidhaa mbovu zisizofaa kwa matumizi ya binaadamu

Makamu mwenyekiti Bodi ya wakurugenzi taasisi ya viwango Zanzibar ZBS Hamisa Mmanga amewataka wajasiriamali na wafanyabiashara kuitumia taasisi ya viwango Zanzibar katika kupata ushauri wa biashara wanazotaka kuzizalisha au kuingiza nchini ili kufuata viwango vilivyowekwa. 

Ameyasema hayo huko Maisara katika maonesho ya 5 ya biashara ikiwa pia ni siku ya kuadhimisha siku ya viwango Zanzibar amesema endapo wataweza kufanya hivyo wataweza kukuza kipato na kupanua soko la bidhaa zao. 

Aidha amewaambia wafanyabiashara kuwa kughushi bidhaa kwa kuweka logo na nembo ya biashara ya mtu mwengine wanapokwenda kuchukua bidhaa kabla ya kuingiza nchini kwani hatua hiyo haipo kisheria. 

Amesema kughushi bidhaa inachangia uwepo wa bidhaa hafifu zisizokidhi viwango hatimae kuletwa bidhaa mbovu zinazoweza kuleta madhara ya afya na mazingira. 

Hata hivyo amesema nchi ya Zanzibar inategemea bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi hivyo kwa sasa IPO haja taasisi ya viwango kuhakikisha wanasimamia na kudhibiti uingizwaji wa bidhaa hizo ili kuhakiki nchi haipati bidhaa mbovu ambazo hazina ubora

“Nchi yetu hatutaki kuwa jaaa la bidhaa mbovu ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu”Amesema Mwenyekiti. 

Akitoa Mada ya maendeleo ya viwango Afisa Viwango Kidawa Hassan Khatib amesema kwa sasa jumla ya bidhaa kumi na saba zimechunguzwa na kuthibitishwa na ZBS kwamba zipo salama kwa matumizi ya binadamu ambapo kumi na moja ni kutoka ndani ya nchi na nne nje ya nchi.

Amesema taasisi hiyo ya viwango itahakikisha inasimamia majukumu yake ili kuleta ufanisi na ubora wa bidhaa hizo zinazoingizwa. 

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanachunguza bidhaa kabla ya kununua ili kuona bidhaa hizo kweli zinanembo ya ZBS au TBS. 

Kwaupande wao wajasiriamali Hadija Mohamed Fadhil na Haji Juma wamesema wanaishukuru serikali kwa kuweka taasisi hiyo ya viwango hapa Zanzibar inayo saidia kutoa sifa na viwango vya bidhaa zao kuuzika kwenye soko la dunia. 

Katika halfa hiyo ya Siku ya viwango Zanzibar taasisi mbalimbali pamoja na wajasiriamali walihudhuria. 

Amina Omar