Bodi ya wazee ya kamati ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya imewataka wasanii kuzitumia fursa za sherehe na matukio mbalimbali kwaajili ya kujitangaza kimuziki Zanzibar na kujipatia kipato.

Akizungumza katika kikao cha wazee wa Bodi kamati tendaji ya chama cha wasanii wa muziki wa kizazi kipya katika ukumbi wa sanaa Rahaleo, Omar Yussuf Chunda amesema kuna fursa nyingi kwa wasaniii wakizitumia vyema kwani wana nafasi kubwa ya kuitangaza nchi.

Aidha amesema wasanii ni watu wanaotumia vipaji vyao kuitangaza nchi hivyo zikitokea fursa wasanii wa kizazi kipya watengenezewe nafasi za kuweza kujitengenezea kipato chao cha kila siku.

“Sanaa ni kitu kikubwa sana na nchi inatangazwa na sanaa ,sisi watu wa Zanzibar tumejaliwa na vipaji hivyo wakubwa wetu waelewe nini maana ya fursa”Alimalizia Chunda.

Kwa upande wao wasanii wa muziki wa kizazi kipya Zanzibar wamesema wapo katika Jitihada za kuifahamisha jamii kuijua thamani yao ambapo wamewataka Wazanzibar kuthamini vitu vya kwao wakiwemo wao wasanii wa Zanzibar.

Rashidi Amini Abdalla (Rico Single) msanii wa Zenj Fleva wa kizazi kipya akizugumza na Zanzibar24 amesema wamekuwa na changamoto kubwa katika kufanya kazi zao kwa baadhi ya watu kutanguliza maslahi yao binafsi badala ya wasanii wa Zanzibar.

“ Zanzibar tumejaliwa na vipaji ila tumekosa uboreshaji na sisi wazanzibar ndio waboreshaji na tuache kukatishana tamaa sisi wasanii wa Zanzibar” Alisema Amini Abdalla (Rico Single).

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Sanaa Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar Dk Omar Abdalla Adam amesema kuna utofauti kati ya msanii wa Zanzibar wa nyumbani na Waugenini, lazima mgeni akija athaminiwe kama vile wao wasanii wa Zanzibar wanavyothaminiwa ugenini.

“Fursa zipo lakini zinataka ufate utaratibu fursa ya kwanza Raisi wa Zanzibar Dk Shein amesaini sheria ya namba saba ya mwaka 2014 ya baraza la sanaa lazima wafate taratibu za kisheria”Alisema Dk Omar  Abdalla.

Aidha amesema wao kupitia Wizara ya sanaa na vijana utamaduni na michezo wapo tayari kushirikiana na wasanii wa Zanzibar kama watakuwa tayari kufanya kazi kisheria inavyotakiwa.