Serikali imesema kuwa manispaa ya mjini itaanza kuwa hadhi ya jiji (jiji la Zanzibar), kuanzia Julai 1 mwaka huu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheir, aliyasema hayo katika ukumbi wa baraza la wawakilishi Chukwani, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Alisema uamuzi huo unakuja baada ya kuridhiwa na serikali katika tangazo la serikali namba 120 la 2015.

Alisema hatua zilizochukuliwa ni kukamilisha maandalizi ya uchaguzi wa Meya, Naibu Meya pamoja na uteuzi wa Mkurugenzi wa jiji atakayeteuliwa na Rais.

Alisema fedha kwa ajili ya uendeshaji wa jiji hilo zitatolewa kuanzia Julai 2019.

Akizungumzia bajeti hiyo, alisema serikali ina mpango wa kufanya utafiti wa kubuni uwezo wa vyanzo vya mapato na udhibiti wake katika serikali za mitaa kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Alisema kufanya hivyo ni kutafuta fursa za upatikanaji wa rasilimali fedha ili kufanikisha utekelezaji wa programu za miradi ya maendeleo.

Alisema katika kuimarisha suala la ukusanyaji mapato katika serikali za mitaa, ofisi yake kwa kutumia wataalamu wa ndani itaendelea kusimamia na kuhakikisha kila manispaa, baraza la mji na halmashauri inakusanya mapato kutoka katika vyanzo vyake vya mapato kwa mfumo wa kielektroniki.

Alisema hadi kufikia Machi 2019, halmashauri zote zimeunganishwa katika mfumo wa pamoja wa ukusanyaji mapato na kuanza kutumia mashine za kukusanya mapato katika maeneo ya maegesho, masoko na vituo vya ukusanyaji ada zitokanazo na usafirishaji wa maliasili zisizorejesheka.

Alisema ofisi ina uwezo wa kuona na kufuatilia taarifa za ukusanyaji mapato kutoka kila halmashauri na kushauri ipasavyo.

Aidha, alisema kwa mwaka wa fedha 2018/2019 mamlaka ya serikali za mitaa zilikadiriwa kukusanya shilingi 12.66 bilioni na kukusanya shilingi 9.10 bilioni sawa na asilimia 72 ya makadirio.