Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imekifunga kiwanda cha kutengeneza dawa za kukosha mikono (SANITIZER) baada ya kubainika dawa hizo hazina kiwango kinachohitajika pamoja na kutokuwa na usajili rasmi.

Hatua ya kukifungia kiwanda hicho kinachojulikana kwa jina la OIL CAM kilichopo Kiembesamaki imekuja baada ya wasamaria wema kutoa taarifa kwa Mamlaka hiyo.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha Vipodozi ZFDA Salim Hamad Kassim amesema kwa hatua ya awali wameamua kukifunga kiwanda hicho na kumpa nafasi mmiliki kufuata taratibu za usajili na kuwasilisha sampuli ya bidhaa wanayozalisha ili ifanyiwe uchunguzi katika maabara yao.

Amesema kawaida bidhaa za viwandani kabla ya kufika kwa watumiaji zinatakiwa zifanyiwe uchunguzi na zifikie kiwango cha ubora unaokubalika kulingana na muongozo  wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuanzia asilimia 75 hatua ambayo bidhaa hiyo haikufikia.

Na Kijakazi Abdalla – Maelezo