Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka waliokuwa wanachama wa CUF kisiwani pemba kutokuwa wanyonge kutokana na kuhama chama walichokijenga na kukitumikia kwa miaka mingi.

Zitto aliyasema hayo jana kisiwani Pemba wakati akizungumza na waliokuwa viongozi wa CUF Wilaya ya Chakechake baada ya kuwakabidhi kadi baadhi yao waliojiunga na ACT Wazalendo.

Alitoa kauli hiyo katika siku ya kwanza ya ziara yake akiambatana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye Machi 18, mwaka huu alijiunga na ACT Wazalendo. Alisema anafahamu wananchi walio wengi hususani kisiwani Pemba wana maumivu ndani ya mioyo yao, lakini hawapaswi kuendeleza maumivu hayo wakijua kuwa safari ya mapambano siku zote hujaa changamoto.

Sambamba na hayo, Zitto amewaka wananchi hao kusimama mstari wa mbele kuendeleza chama hicho bila ya kukubali kuchokozeka na anaamini misukosuko mingi itajitokeza.

Alisema ipo haja ya kila mtu kufanya kazi ya ushawishi kwa wingi ili walio wengi waendelee kujiunga na ACT hatimaye washinde katika uchaguzi wa ujao 2020.

Mratibu wa zamani wa CUF- Pemba, Said Ali Mbarouk alisema kwenye kisiwa hicho yaliyokuwa matawi ya CUF yamegeuka kuwa ya ACT na wanasubiri baraka za uongozi ili harakati ziendelee.