WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Issa Haji Ussi Gavu, amewataka vijana wa taasisi ya itifaki,upatanishi na huduma za umma (ZPNS), kuendelea kulenga pamoja  kwa kufikiri na kuweza kuamua pamoja ili lengo la kuundwa kwa taasisi yaoliweze kufikiwa kwa wakati.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika sherehe ya kutimia mwaka
mmoja tokea kuasisiwa taasisi hiyo yenye lengo la kuweza kutatua migogoro ikiwemo upatanishi pamoja na utoaji huduma kwa umma.

Alisema haitokuwa fahari wala faraja kuona kuwa taasisi yao hiyo inagawanyika kwa msingi wowote, ambapo mategemeo ya serikali mgogoro unaowakuta wataweza kuutatua kwa kuupatia suluhu bila ya kuvunja umoja huo.

Aidha alisema kuwa itakuwa jambo la kushangaza taasisi yenye lengo la kushughulikia  migogoro yao ikawa ina migogoro kwani itaweza kuipatia sifa mbaya taasisi yao na kurejesha nyuma malengo yao.

“Nna hakika taasisi hii itakuwa kwani mumeweza kuwafanya vijana mwengine wawe na mwamko wa kuwakusanya wenyewe taaluma moja ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza siku hadi siku” alisema.

Alisema kwa kweli taasisi hiyo imeonesha utayari na upeo wao wa kuunda
taasisi hiyo kwa kuweza kuwaunganisha vijana hao ili kuweza kujiajiri bila ya kumtegemea mtu.

Aidha alisema kuwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo pia wataweza kupaza Sauti zao na kuweza kusikika zaidi kuliko kuwa mmoja mmoja.

“Zipo taaluma zinazoweza kujitegemea mtu mmoja mmoja ikiwemo, daktari, uhandisi na mwanasheria, uhasibu ila kwa upande wenu hamukujiona mkwa hivyo kwani mumeona haitoleta tija kubwa na ndio maana mukaona mujiunge pamoja ili tija ipatikane kwa hilo hongereni sana” alisema.

Hata hivyo aliipongeza taasisi hiyo kwa mafanikio waliyoyapata ikiwemo kuendeleza kuwepo na kuweza kufanya kazi kwani kumekuwepo taasisi nyingi zinaanzishwa halafu zinakufa kwa sabaabu tofauti ambapo huwa zinapoteza malengo ya kuanzishwa kwake.

“Kwa kweli ni jambo la kupongezwa sana kuanzisha taasisi kisha mukafikia wakati mukajipongeza kwani ni kitu rahisi kumekuwepo taasisi zinaanzishwa hazifiki muda zinakufa ila kwa ZPNS hongereni kwa hili”alisema.

Sambamba na hayo aliitaka taasisi hiyo, isiishie kwenda kutoa huduma katika masuala ya itifaki pekee bali wajikite pia kutizama fursa ya kuweza kutoa vifaa vikavyowezesha mikutano wa kitaifa nchini wakiwa ni miongoni mwa watu wanaofanisha mikutano hiyo.

Nae mshauri wa taasisi hiyo, ambae pia ni Mkuu wa mkoa wa mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema, tokea kuanzishwa kwa taasisi hiyo imekuwa inapatikana faraja ya uwepo wa taasisi hiyo kwani mara nyingi zinapotekelezwa shughuli mbalimbali vijana hao imekuwa ni
watu wa kwanza kujitolea katika shughuli hizo.

Aidha alisema shughuli hizo ni moja ya nyenzo muhimu ya kutekeleza shughuli kwa mujibu wa taratibu zinazotakiwa kwani sio watu wengi wanaofahamu na kujua umuhimu wa suala la itifaki.

“Wengi tumezowea tunafanya jambo letu kikawaida tu ila kwa wenzetu hawa waliosoma na kuzowea kufanya jambo la itifaki kwa muda mrefu tunaona wakati wote wanatumia itifaki katika kutekeleza majukumu yao hivyo muendee kueneza kazi yenu kwa moyo” alisema.

Sambamba na hayo alisema kujikusanya kwa vijana hao, ni muono wa vijana ambao wamekuwa wakiona mbali kwani kumekuwepo mabadiliko makubwa ya  dunia kwa sasa na nchi ya Tanzania ni moja wapo ya mabadiliko hayo.

Hivyo aliwataka vijana hao kutovunjika moyo na kuendelea kufanya kazi zao kwa vitendo ili huduma ziweze kupatikana kwa wakati uliopo.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Omar Habib Omari, alisema kuwa taasisi yao ipo Zanzibar na Tanzania kwa jumla ambayo lengo lake ni kufanya shughuli za itifaki, upatanishi na huduma za umma sambamba na kuona vijana waliosoma masuala ya kimataifa na diplomasia wanaunganisha nguvu zao kwa pamoja na kuweza kutoa mchango wao ikiwemo usuluhishi wa migogoro.

Akitoa neno la shukrani katika Hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Abdallah Juma Sadala, alisema Chama kimefarijika kuona vijana hao wamejiunga pamoja na kuweza kufanya kazi zao za kiitifaki katika nchi sambamba na kuahidi kuwa Karibu nao kwa kuwaunga mkono ufanyaji wa kazi zao za kila siku.