Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) imetiliana saini na Kampuni ya nchini Norway Mkataba wa Uanzishwaji wa mfumo wa Mashine za kielektroniki za kutolea risiti ili kuimarisha huduma ya ukusanyaji wa mapato Nchini.

Akizungumza  baada ya utiaji saini huo katika ukumbi wa bodi hiyo Mazizini Mjini unguja, Kamishna wa ZRB Joseph Abdalla Meza, amesema mfumo huo utaisaidia ZRB kukusanya mapato kwa urahisi pamoja na kuwatambua wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi za Serikali.

Amesema kuna baadhi ya Wafanyabiashara wamekuwa wakikwepa kulipa kodi kwa kutowapa wateja wao risiti za halali na kusababisha baadhi ya  mapato ya serikali kutokusanywa ipasavyo.

Kamishna Meza amesema mashine hizo zitakuwa na uwezo wa kutoa taarifa za wafanyabishara kulingana na Biashara wanazoingiza Nchini bila ya kufanya Udanganyifu wakati wa mauzo.

Amesema kuanzishwa kwa mashine hizo kutarahisisha upatikanaji wa kodi pamoja na kutapunguza migogoro kati ya Wafanyakazi wa ZRB na wafanyabiashara wakati wa ukusanyaji wa mapato.

Aidha amesema pia Mfumo huo utapoanza kufanya kazi pia utaweza kuondoa tatizo la Rushwa kwa wafanya biashara kutoka na kukusanya taarifa kwa njia za kielektronik  ambazo zitatowa ripoti kamili za wafanya biashara wanaolipa na kutoa risiti kwa wateja wao.

Aidha amechukuwa fursa hiyo kuwataka wananchi kuimarisha mashirikiano juu ya kudai risiti wanapo nunua bidhaa zao ili kuchangia ukuwaji wa Maendeleo Nchini.

kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji  wa Kampuni ya Norway Registers Development (AS) ,Mindaugas Glodas amesema mfumo huo ukitumiwa ipasavyo utaweza kusaidia ZRB kukusanya kodi kwa urahisi kwa wafanyabiashara wote.

Amesema mataifa mbalimbali yamekuwa yakitumia mfumo huo kwa kukusanya kodi kwa njia ya kielektronik ambayo ni rahisi kukusanya mapato ya Nchi.

Aidha amesema Kampuni yake itaendelea kushirikiana na Bodi ya Mapato Zanzibar ZRB ili kufikia malengo waliyoyakusudia katika kuimarisha huduma za kijamii kupitia Kodi za Nchi.

Mfumo huo unatarajiwa kuanza rasmi baada ya miezi sita ambapo  wafanyabiashara wote wa Zanzibar watalazimika kutumia mfumo huo katika kulipa kodi na kuhifadhi taarifa zao za mauzo na manunuzi ya bidhaa.

Na:Fat-hiya Shehe Zanzibar24.