Jumla ya wastaafu elfu tisa wanatarajiwa  kuhakikiwa taarifa zao na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii  Zanzibar ZSSF katika muda wa siku 9 kuanzia leo Julai mosi.

Akizungumza na waandishi wa habari Afisa Uhusiano na Masoko kutoka ZSSF  Mussa  Yussuf, wakati  wa zoezi hilo lililofanyika katika uwanja wa kufurahishia watoto karikaoo wilaya mjini amesema uhakiki huo unafanyika Unguja, Pemba na Dar-es-Salaam kwa muda wa siku 9 na unatarajiwa kuwafikia wastaafu zaidi ya elfu 9.

Afisa Uhusiano na Masoko ZSSF  Mussa  Yussuf akizungumza na vyombo vya habari

Ndg. Mussa ameeleza kuwa zoezi hilo la uhakiki kwa mwaka huu limekuwa tofauti na miaka mingine kwa kusogeza huduma hiyo kila wilaya ambapo kwa Mkoa wa mjini  linafanyika katika kiwanja cha kariakoo, Mkoa kaskazini linafanyika katika kiwanda cha sukari Mahonda na Mkoa Kusini linafanyika Dunga .

Kwa upande wake Afisa habari Mwandamizi kutoka ZSSF Raya Khamisi amesema ZSSF imeamua kusogeza huduma hizo ili kupunguza msongamano wa watu na kuwapunguzia usumbufu wazee hao katika zoezi la uhakiki na kuchukua tahadhari kubwa ya ugonjwa wa Corona.

Nao baadhi ya wazee waliofika kufanyiwa uhakiki katika vituo wamesema kwa sasa zoezi hilo limekuwa na ubora zaidi kutokana na kuwaondolea usumbufu baadhi ya wazee ambao wanaotoka mbali na maeneo ya Mjini .