MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imewataka wafanyabiashara wanaouza mafuta ya petroli na dizeli sehemu zisizo rasmi, kuacha tabia hiyo kwa sababu ni kosa kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Chake Chake, Mkaguzi wa mafuta kutoka ZURA ofisi ya Pemba, Abduladhim Ridhiwani Mohamed, alisema, kuna baadhi ya watu wana tabia ya kuuza mafuta vichochoroni, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha yao na  watu wengine.

“Tutatoa vibali kwa watu maalumu tu kama wavuvi ambao huchukua mafuta na kwenda kuingiza kwenye mashine zao za boti, lakini kwa wengine wanaouza nje ya vituo hatutawaruhusu kufanya hivyo,” alisema.

Pia aliwataka wenye vyombo vya moto kununua mafuta kwenye vituo vya mafuta, kwani ni salama.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano, Huzaimat Bakar Ali, aliwaomba  wananchi kudai risiti wanapokwenda kununua mafuta, ili linapotokea tatizo waweze kufika sehemu husika na tatizo lao kupatiwa ufumbuzi.

Akiwasilisha mada, Ofisa uhusiano kutoka ZURA, Hassan Juma Amour, alisema dhamira ya mamlaka hiyo ni kusimamia huduma za nishati na maji kwa uwazi na ufanisi, ili kukuza uwekezaji na kuchangia maendeleo ya kiuchumi Zanzibar.

Akielezea mafanikio waliyoyapata tokea kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ni pamoja na kuhakikisha mashine za kuuzia mafuta ziko sahihi, kutoa miongozo ya kuimarisha vituo vya mafuta pamoja na kufanya ukaguzi katika vituo na bohari za mafuta.

Hata hivyo, alisema bado kuna  uwelewa mdogo juu ya majukumu ya ZURA kwa taasisi zinazodhibitiwa na jamii kwa ujumla.

Mapema akifungua mkutano huo, Ofisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Juma Bakar Alawi, aliwaomba  waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuielimisha jamii hususani udhibiti wa nishati na maji, ili kuepusha migogoro.

Nao waandishi wa habari, walisema wamefarajika kupata mafunzo hayo, kwani wamejifunza vitu mbali mbali, ikiwemo taratibu za kutoa malalamiko na pamoja na majukumu ya ZURA.

Mkutano huo wa siku moja uliandaliwa na ZURA lengo likiwa ni kwenda kutoa elimu kwa jamii, ili kuepusha migogoro.